KISWAHILI NI KIKONGWE

Leo ningependa kuwavulia kofia watangulizi wetu. Waliopo na wasiokuwepo. Wenye uhai na wasiokuwa na uhai tena. Kwa kututangulia katika maji haya male ya kiswahili. Ama kwa kweli kama si nyinyi tusingepata leo msingi wa kufurahia utandawazi tulionao wa kiswahili kwa hivi sasa. Nyie mmekuwa mhimili ambao sie tumepata nguvu za kustahimili makuu na madogo. Licha ya kwamba ulimwengu huu umekengeuka na hata kiswahili kimekengeuka, bado maadili yenu ya lugha mliokakania na kungangania yatabaki mioyoni mwetu daima dawamu.

Nisipomtaja maalim mwendazake Sheikh Shaban Robert kwa kutukunjulia jamvi zuri la simulizi bora za kiswahili sijui nitamtaja nani! Maandishi yako Ustadh kama vile ” Adili na Nduguze” , Kusadikika, Utu Bora Mkulima na mengineyo yamekitav mizizi katika mioyo yetu na kuyang’oa mtu hawezi.

Hivi karibuni nchini Kenya tumempoteza mwandishi wa vitabu vya kiswahili, kijana mdogo sana marehemu Mrono Eliud. Mola airehemu roho yako mahali pema panapokufaa swahiba Mrono. Mchango wako katika lugha ya kiswahili utaandikwa katika mioyo yetu kwa wino usiofutika. Juzi juzi tu ustadh Shuara, mzee wetu mzima tuliyekulaza kwenye nchi bora ya Ukambani-Matuu umetutoka. Urithi wako ulioturithisha siku ile tumekutembelea ungali unatufaa pakubwa.

Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, wewe ni Gwiji na Bingwa aliye hai na tunayefaa kujivunia kwa majivuno kila leo bila ya haya wala izara yoyote. Ulitufufulia Ngeli bora za Kiswahili zilizokuwa zimezikwa kwenye kaburi la Mzee Kapinga. Nani kama wewe Mzee? Nakuombe a maisha marefu yenye utuvu na utulivu wa kipekee!

Tokea pwani za Kenya na Tanzania kiswahili chetu kiliumbwa, miaka ile ya nyuma kwa nini tukiumbue katika miaka hii ya mbele? Mbali kitokako kiswahili chetu na mbali kiendako hivyo basi hatuna budi kukitetea vikali.

Siku moja nikisafiri kwenye matwana, nimejipata nikiwa na darasa nisilolipangia. Alikuwa amenipigia simu rafiki yangu  kwa rununu yangu nami kwa desturi na kaida nikamjibu kwa ufasaha na uketo wa lugha nisijue kwamba hadhira nimeipata. Wenzangu matwanani walitilia maanani vyote nilivyosema na hata wengine wakapitishwa stani zao wakisikiliza hadithi zangu tu ambazo hazikuwahusu ndewe wala sikio. Kwa nini? Sababu kuu ni kuwa sote tunafurahia kiswahili kikizungumzwa kwa ufasaha na  kwa hivyo hatuna budi kukizungumza pia kwa ufasaha ili wengine wakifurahie na watambue kwamba  ama kwa kweli kiswahili kipo.

Tumo kwenye karne ya ishirini na moja na mwito wangu kwetu sote ni kukitumia kiswahili kwa njia zote tuwezazo kwani ni muhimu kuenda na wakati ili tusipitwe na wakati uo huo. Zaidi ya yote tukumbuke kwamba kiswahili ni kikongwe.


11 Responses to “KISWAHILI NI KIKONGWE”

 1. Wapi tena kama soi nyumbani East Africa, huku ndiko wagwiji wa lugha wanazaliwa, huku ndiko waswahili hawa wanakomaa katika talanta yoa ya uswahili. Ndiposa inatubidii tuwasaluti na kuwapa shukrani kwa matoleo ya kwa lugha hii: Ken Walibora, Katama Mkangi, Alamin Mazrui, Z burhani, Ngugi wa Thiongo n.k

  Like

 2. Ama kweli kumbukumbu za weledi wa Lugha ya Kiswhili,waliotutangulia, hazitawahi kufutika kamwe kwenye mitima ya wapenzi wa kiswahili. Waliweza kukunjua jamvi la Kiswahili, hadi upeo fulani, lakini bado nampongeza mwalimu Msonobari kwa kuendelea na kazi si haba ya kuzidi kulikunjua jamvi hilo na kukienzi Kiswahili vyema kabisa. Sina budi kumvika swahiba huyo pete, maana yake, ‘chanda chema huvikwa pete’. Nasi pia wanafunzi na wapenzi wa Kiswahili, tuzidi kikitilia zingatio na kukiinua Kiswahili hadi upevuni. Asante.

  Like

 3. Namvulia kofia mwalimu msonobari kwa kuienzi lugha hii.

  Like

 4. Kiswahili ni kikongwe. Mwaka 1963 kupitia kwa lugha ya Kiswahili wakenya walijipatia uhuru. Wote waliotuaga akiwemo bw. Eliud Mrono, Katama Mkangi na wengineo Mola azilaze roho zao mahali pema peponi. Kazi itabaki kuwa rotuba kwa wapenzi wa lugha ya kiswahili. Shukrani bingwa. STEPHEN MUKANGAI, KIMT.

  Like

 5. Nami nakuvulia kofia bingwa. Ukweli ulio wazi kama mchana wa jua ni kuwa kisima cha zamani hakifunikwi. Ndugu zetu waliotuaga, na Mungu ahifadh roho zao mahali pema peponi. Ni pigo kubwa sana kwa taifa hili kuwapoteza watu kama hao. Tulio hai na tufuate nyayo zao. Hapana shaka kwamba wameacha nyayo zao katika safu ya wangoi. Kiswahili ni kikongwe, na ina maana kuwa kina utukufu ulio kita mizizi. STEPHEN, KIMT.

  Like

 6. Naamini kwamba wapenzi wa lugha ya kiswahili wanayo kila sababu ya kujivunia blogu hii, kwani wanapata fursa ya kipekee ya kujua mengi kuhusiana na historia ya wale wakongwe ambao wametutangulia mbele za haki. Wao ni mashujaa wetu. Kiswahili kitukuzwe na kisifukuzwe.

  Like

 7. Kwa maana hiyo tunalojukumu la kuwakumbuka wakongwe wa kiswahili. Walio tuaga MOLA azihifadhi roho zao mahala pema peponi.

  Like

 8. Kiswahili kinahistoria ndefu na safi.

  Like

 9. Swadakta ndugu yangu! Kiswahili na Waswahili kama wewe wapo kwa wingi. Masikitiko ni kuona wengi wetu wanakionea Kiswahili haya. Wamesahau kuwa Kiswahili ki kitamu!

  Like

 10. Ninakihenzi Kiswahili.Kimekuwa lugha ya kimataifa.

  Like

 11. Wah kakah mtanange wako si wa kuangalia na macho ya upekuzi nakuvulia kofia kaka

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: