KISWAHILI JIJINI NAIROBI

Sijui kama umewahi kutembelea jijini Nairobi  kwa maana kama umewahi, basi utakubaliana na mimi kwa asilimia mia moja na moja. Kama hujawahi basi pana uwezekano kwamba hutanielewa fika nitakachokuwa nikizungumzia leo.

Mjini Nairobi, shughuli ni kabambe na kila mtu yu mbioni!

Mara yangu ya kwanza nimelizuru jiji la Nairobi, nilikula mwande kweli kweli.

Nilikokuwa nikienda sikukufahamu vizuri. Kila nilipojaribu kuulizia njia, nilitazamwa kwa macho ya upekuzi, na kuonekana mpuzi, asiyejua anachotaka maishani. Hatimaye, niliijua njia ya kwenda kule nilikokuwa nikienda lakini si kwa kuelekezwa bali kwa kupotea. Wenyewe husema, kupotea njia ndiko kujua njia. Nilipouliza nikaambiwa, ‘Enda uko bere uurizie uko. Mi sijui.’

Siku nyingine nimesimama kando ya jengo la Hilton, karibu sana na duka maarufu la viatu la Bata. Kitu ambacho lazima nikiri ni kwamba, mji huu umeshehenezewa warembo na watanashati chungu nzima. Sasa pale nilipokuwa nimesimama, nimezungukwa na warembo kadhaa. Wamejitia hamnazo na kunivalia miwani ya mbao. Hawanioni! Kumbe urembo wa sura si urembo wa salamu, mawasiliano na hata utu. Kila nikijaribu kumsalimia huyu na kumjulia hali tu, ananitazama utadhani nimetangazwa kwenye habari kuwa mimi ndimi gaidi linalotafutwa. Kwetu nitokako, sikuzoea hivi. Nilipojaribu kumsifia alivyokuwa akipendeza bila nia yoyote mbaya, akasonya na kuniambia, ‘Esh, tebu niache we! Kwani unaashwa na nini? Mi unanijua?’

Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nikihisi njaa sana. Rafiki yangu mmoja Mkenya, kwa jina Emmanuel Mokaya, alikuwa amenielezea kwamba samaki mzuri pale jijini ningempata katika mkahawa uitwao Kosewe. Basi, saba kamili ilipofika, nilijipata nimeketi ndani ya mkahawa huo, namwita mhudumu kunihudumia. ‘ Za saa hizi dada?’ ‘Eeeh! Unasemaa,’ Ndilo jibu nililopata katika majaribio yangu ya kuanza kuagizia chakula. Nilimezea hayo kwa njaa niliyokuwa nayo, na kumwambia, ‘Naomba samaki wa kuto…’ ‘Hapa tunauza hatupeani bure!’ ‘Sikiza dada, hela ninazo, lakini naomba samaki wa kuto…’ ‘Samaki wa kutoka wapi! Hapa hatuna samaki wa kutoka mambasa. Samaki yetu inatoka Kisumo.’ Nikawa karibu napandwa na wa kwangu. Maana ilikuwa wazi kwamba hatukuwa tunawasiliana. Njaa niliyokuwa nayo ilinishangilia kuanzisha ugomvi na dada mhudumu yule lakini maadili na uungwana wangu, vyote havikuniruhusu. Nikiwa bado nayafikiria hayo, dada alinitoweka utadhani alikuwa ameliona jini au ziraili. Bahati yangu, mzee mmoja wa makamu, aliyeshuhudia yote hayo, alinijia na kuomba kunisaidia. Hatimaye aliniletea samaki wangu wa kutoswa kwa sima moto na  sharubati baridi ya embe. Baadaye niligundua kwamba ndiye aliyekuwa mmiliki wa hapo.

Msonobari akiwa mkahawani akifurahia mlo wake hatimaye!

Siku nyingine nikiwa stanini nikirudi zangu nyumbani, nilisikia utingo akisema, ‘Beba mmoja, beba mmoja.’ Basi moja kwa moja nikajibwaga ndani kuelekea kwa mwenyeji wangu kule Lang’ata. Baadaye tukaanza mwendo. Wakati utingo anachukua nauli, nikamwambia nitashukia Uhuru Gardens, Lang’ata. Hapo ndipo alipopaza sauti na kuniambia, ‘ Sisi tunaenda Umoja.’ Kwa kilio na uzushi, nikamwambia, ‘ Hukusema beba mmoja ndugu yangu? Kwamba bado mmoja gari lijae?’ ‘We wacha kutusumbua. Kama hujui kule unaenda, jipange. We dere, shukisha huyu mtu.’ Kwa kweli nilishushwa huku nikishusha pumzi nzito kwa masikitiko na mapukutiko.

Baada ya kushushwa kwa lazima nilishusha pumzi nzito na kurudi tena stanini

Sina muda leo, lakini nikipata tena, nitawaelezea zaidi matukio ya Kiswahili  yaliyonitukia jijini Nairobi. Lakini katu sitoki humo jijini Nairobi kwani ndimo kazi ya Kiswahili inamohitajika zaidi  na mgalla mwue na haki yake umpe.


16 Responses to “KISWAHILI JIJINI NAIROBI”

 1. Ama kweli weledi wa mambo hawakuwa wakipaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walipopanua vinywa vyao vyenye busara, waliponena ya kuwa, ‘ akili ni nywele na kila mtu ana zake.’ Hongera mwalimu Msonobari kwa utafiti wako wa kukomboa kizazi chetu kipya. Inadhihirika wazi kuwa, mja yeyote akikuona ukitembea asidhani ni ziara tu, bali ni utafiti unaofanya ili kuboresha lugha teule ya Kiswahili, Jijini Nairobi watu wengi wamekipotosha Kiswahili sana. Lakini kwa rehema na nehema zake Manani, tushampata mjuzi wa lugha Mwalimu Msonobari kutuelekeza, shukrani kwa utenda kazi wako mzuri. Rabuka akujalie maisha marefu. Asante sana.

  Like

  • Wallahi nina furaha iso kifani kwa kuiona jitihada, ya kaka Msonobari kuhusiana na juhudi yake ya kutaka kuuamsha utamaduni wetu ambao ni Kiswahili. Kwa muda mrefu wasomi wameshindwa kujieleza kwa Kiswahili hata viongozi kama mawaziri na hata maraisi waliowahi kuiongoza Kenya wanakibambanya Kiswahili. Hakika na shangazwa na Wakenya wapi twaelekea. Kiswahili tumrekibeza tukakichanachana mpaka sasa hakituunganishi kama Wakenya. Kiswahili ni kitukuzwe tukitaka kuuwa ukabila Kenya.

   Like

 2. Nairobi, mji wenye masaibu mengi na kwa asilimia mia moja nakubaliana nawe! Pole kwa hayo lakini kama tu vile miji mingi inayokua duniani, Nairobi ni jiji lenye watu wenye hulka tofauti kama ardhi na mbingu! Niamini, hata salamu Nairobi zinauzwa! Lakini tupo, twaishi!

  Like

 3. Ziara yako ya jijini Nairobi imenipa mseto wa hisia ya furaha na huzuni. Nairobi ni “mji wa mawe” wasemavyo wenyewe. Muungwana akivuliwa nguo huchutama, ujumbe wako kupitia kwa blogu hii ni changamoto kwa wakaazi wa jiji la Nairobi. Iwapo wao ni waangwana, basi watachutama. Kwa upande wako bingwa nakusihi tafadhali usibanduke jijini Nairobi. Wewe tabibu wa aina yake ambaye anaouwezo wa kupima na kutibu ugonjwa wa wa jiji hili kuu la Kenya. Ganga ganga za jabara humuacha mgonjwa na matumaini ya kupata nafuu. Hongera kaka Msonobari, na vilevile pole sana kwa mapokezi mabaya uliopewa na wakaazi wa Nairobi. STEPHEN, KIMT.

  Like

 4. Ustadhi, ni ukweli mtupu kuwa sura nzuri yaani urembo na utanashati bila ukarimu, uungwana na nidhamu ni sawa na ibaada bila sadaka. Hapo nakubaliana nawe asilimia mia na moja. Lakini kupitia kwako Mola atawageuza. Heko galacha. Nyuma usirudi, mbele endelea. STEPHEN, KIMT.

  Like

 5. POLE kwa masaibu hayo yote uliyoyapitia NAIROBI.ama kwa hakika ni jambo la fedhea kuona jinsi wengi wameibagua lugha yao asili huku wakizidi kupotoka maadili.TUKIENZI kiswahili na bila ya shaka yoyote kitazidisha ushikamano aushini mwetu,KAKAVINNIE,KIMT

  Like

 6. Katika jiji la na Nairobi watu wamo mbioni, kila mmoja ana bahasha kubwa mkononi kutafuta ajira. Utafiti wangu umenonyesha kuwa wengi ambao wanaangaika, hawapendi Kiswahili. Ni vigumu sana kupata mpenzi wa kiswahili anapiga lami. Tafakari hayo. Stephen, Kimt.

  Like

 7. Kwanza mie na toa pole zangu kwa yale yaliyokupata katikati ya jiji la Nairobi wala si mwa Nairobi,jiji ambalo halina utu na lililo sheheni ubinafsi.Ni nadra sana kuwapata wapenzi wa lugha jijini humu.Kila napzungumza Kiswahili bora na si bora Kiswahili wenzangu huniambia Kiswahili kitanifaidi nini.Kingereza kimependwa sana na ajabu ni kuwa walungao huvurugha lugha ya wenyewe.Ni lini tutajifunza kujivunia kilicho chetu? Titi la mama li tamu sana na chako ni chako kikioza kikaushe.

  Like

 8. GALACHA, mvumilivu hula mbivu. Naamini matunda ya uvumilivu wako sasa unayachuma. Uliokumbana nayo jijini Nairobi, ni dhuluma tupu. Lakini jambo la muhimu ni kuwa ulivumilia. Naamini kuwa ushuhuda wako ni changamoto kubwa kwa wakazi wa jiji la Nairobi. Shukran ustadhi. STEPHEN, KIMT.

  Like

 9. Japo ulokumbana nayo jijini Nairobi ni ya kutamausha’hongera kwa uvumilivu wako,kama ulivyo wasitiri baadhi ya wenyeji wa jiji hilo maulana naye atakustiri.ustadh kazi yako ni kazi inayo stahili pongezi endelea kuelimisha walo wengi ukizingatia kwamba kila jambo jema ni sadaka na zetu ni pongezi lakini daraja kuu ya malipo iko kwa mola ‘Rabi zidna ilm wa ruzukuni faham.inshallah.mwanasha Gaserego,mwanafunzi kimt.

  Like

 10. Ustadh, pole kwa yalokufika. Jijini Nairobi hapana ukarimu. Mwalim karibu sana kwetu. Mercy wa KIMT.

  Like

 11. Hali ya jiji la Nairobi ni mbaya sana hususana matumizi ya lugha ya kiswahili ambayo yamehathiriwa pakubwa na matumizi ya mtindo wa sheng. Tafadhali bingwa tusaidie katika vita vyetu dhidi ya jinamizi hili,

  Like

 12. Jiji la Nairobi lina mitaa mingi ambayo kwa pamoja imebuni lugha ya mitaani. La kuhofia ni kwamba hata viongozi wetu wamo ndani. Tafadhali nawaomba wakaazi wa jiji hili kutilia mkazo lugha ya taifa. kongole Ustadhi.STEPHEN KIMT

  Like

 13. Heko ustadh Msonobari kwa juhudi zako az kuikuza lugha kiswahili jijini Nairobi, kwani siku hizi wakazi wa Nairobi wameonyesha bidii yao ya kuiendeleza lugha ya kiswahili kwa kuandaa na kuhudhuria makongamano.

  Like

 14. Siku hizi inaitwa Nairobbery.

  Like

 15. Bwana Msonobari naridhika na maelezo yako kifasaha nahisi nikiwa jijini humo kushuhudia uliyojabikia,kweli kwa hali na mali hata kama ni kwa rukwama kiswahili hakitakwama kitafika mbali bila ubishi,Hobee!!!!

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

 
%d bloggers like this: